




Wakati mwingine tunajikuta tumo katika hatari ya kimaisha. Ndio maisha. Ijumaa ya tarehe 6 ya mwezi huu wa Novemba nililala kijijini Tungamalenga, Idodi, Iringa. Tunaweza kabisa kusema kuwa, si tu kijiji hiki kinapakana na mbuga ya Wanyama ya Ruaha bali kimo ndani ya mbuga hiyo kutokana na mazingira yake yalivyo na hususan jinsi wanyama walivyo karibu kabisa na kijiji hicho.
Jioni ile ya Ijumaa ya juma la jana nikiwa na kamera yangu begani niliamua kuzunguka kijijini na kuongea na baadhi ya wanakijiji. Hivi ni nini kero kubwa ya kijiji hiki? Nilimwuliza kijana Hussein Abdalah, fundi Seremala na mkulima kijijini. Hussein ambaye hakusita kuniambia kuwa hukata ' kiharamu' miti ya mbao ndani ya mbuga ya Ruaha alionekana kuwa mwenye taarifa na maarifa mengi katika mazingira wanamoishi.
" Braza sisi hapa kijijini hatuna ugomvi na simba, tuna ugomvi mkubwa na tembo na wanalindwa na Serikali. Ukimwua tembo mmoja ni faini ni zaidi ya milioni tano. Kwa kifupi tembo hasa wakati huu wa kiangazi na ukame wanaingia kwa makundi kwenye mashamba yetu. Wakiingia shambani kwako wanafyeka kila kitu kwa maana ya kula. Wanakula matikiti, nyanya, mahindi, mpunga, yaani hawa jamaa zetu hawaachi kitu shambani. Sasa tikitoa taarifa kwa watu wa TANAPA tunaambiwa fidia ya Serikali ni laki moja kwa eka! Na bado mkulima anaambulia elfu ishirini tu kwa eka, nyingine jamaa wanatia mfukoni." Kijana Hussein alinisimulia kwa masikitiko.
Nilimwuliza tena; " Tatizo ni tembo tu?" Akanijibu.
" Ndio hivyo braza, ugomvi wetu sisi ni tembo tu, kama itatokea vita hapa, basi itakuwa ni vita kati yetu na tembo. Simba hatuna matatizo nao hata kidogo. Wanakuja kijijini mara kwa mara. Lakini huwezi kusikia simba kamtafuna mbuzi au ndama. Wakija shida yao ni maji ya kunywa tu."
Kijana Hussein akawa tayari kunipeleka pori la jirani hapo kijijini nijionee mwenye njia wanayopita tembo na hasa muda huo wa jioni wakati giza likikaribia. Ilishatimu saa kumi na mbili na nusu jioni. Hussein na mimi tukaanza kuliingia pori kwa miguu. Wahenga walinena; " Usivamie pori kwa wembe!'. Mimi hata wembe sikuwa nao, nilibeba kamera tu! Hussein naye hakuchukua chochote. Hussein aliniambia hatutakwenda umbali mrefu porini kabla hatujaona miguu ya tembo na mavi yao. Kumbe, tuliingia porini zaidi ya nusu kilomita tukifuata njia ya tembo. Niliona miguu na mavi ya tembo, mengine yalikuwa ni ya jioni ya jana yake, bado yana ubichi. Na ghafla ndipo nikasikia mlio wa ' tarumbeta' za tembo. Nikamwambia Hussein tugeuze turudi.
" Hapana braza, wanaokuja mbele yetu ni tembo wasiozidi kumi. Wamevuta harufu yetu. Ni kutokana na upepo. Tunachotakiwa kufanya ni kuingia zaidi porini upande wa magharibi. Tuzunguke nyuma yao. Vnginevyo, wana kasi, watatufikia kabla hatujafika kijijini." Nilifahamu pia, silaha kubwa tuliyokuwa nayo ni mikono yetu. Tembo akikukaribia unachotakiwa ni kupiga makofi kama unamshangilia, naye atakimbia. Lakini hutakiwi kupiga kelele ya mdogo au kupiga honi kama umo garini. Mlio wa honi unafanana na mlio wa ' tarumbeta' ambao tembo hutoa. Tembo akisikia mlio wa honi huhisi kuna tembo mwingine aliyeingia katika ' domain' yao, ni adui. Hapo tembo anaweza kukupondaponda na kukuzika ardhini hata kama bado uko hai.
Katika hali hiyo nilifahamu, kuwa sikutakiwa kuwa mbishi bali ni kufuata maelekezo ya Hussein aliye na uzoefu zaidi wa pori lile la Tungamalenga. Tukachota zaidi pori kufuata mwelekeo wa magharibi. Ikanijia hofu kuwa tunafanyaje tukikutana na kundi la simba. Hata kama naweza kuparamia mti wa karibu lakini simba wa Ruaha wanafahamika kwa uwezo wao wa kuparamia miti. Nilihisi kifo hakiko mbali sana. Nilimwuliza Hussein wa sauti ya chini;
" Vipi tukikutana na ' masharubu'?" Simba haitwi simba porini.
" Sharubu hana tatizo. Ikitokea cha kufanya ni kutulia tu na kupita mbali naye huku tukimwangalia. " Nikafikiri kuhusu nyati pia. Lakini najua kuwa nyati walio kundini hawana tatizo, tatizo ni nyati aliye peke yake. Na kama atanikimbiza, cha kufanya ni kukimbia na kisha kuanguka kifudifudi na ' kujifanya' nimekufa. Ataishia kunilamba nguo zangu, anaweza kuzichana na labda kunichubua na ulimi wake. Mwisho nyati ataniacha kama nilivyo. Inahitaji 'kumeza barafu tumboni'. Utulie baridi na kupumua kwa mbali.
Kwa mbali tuliona vumbi likimtimka kutufuata. Iliashiria kundi lile la tembo lilishatupita. Nasi, tuliweza kulifuata nyuma kurudi kijijini Tungamalenga. Nyuma kabisa katika kundi lile la tembo kulikuwa na 'tembo mzee'. Alitembea polepole, hata kama tungekuwa nyuma ya tembo wale kwa mita kumi bado wasingepata harufu yetu. Ndio asili ilivyo. TAHADHARI: Usijaribu kutembea kwenye pori lenye wanyama wenye kudhuru kama huna mwenyeji wa eneo hilo, na zaidi uwe na maarifa ya msingi ya kukabiliana na hatari ya porini.